Washirika Nashukukuru
Ukaraguni • Shukrani

Washirika Nashukukuru

Tarehe: Mei 30, 2013 - Kimani wa Mbogo

Washirika Nashukukuru

Kwa hili langu shairi, nina mengi kueleza,
Ni mengi yaliyojiri, kufadhili mkaweza,
Nawasifu kwa mazuri, kwa wingi kujitokeza,
Washirika nashukuru, mlinifaa pakubwa.

Shukurani kina mama, kuniombea Mwenyezi,
Kutenda hamkukoma, mlitenda kwa uwazi,
Nawaombea neema, Yesu awe kiongozi,
Washirika nashukuru, mlinifaa pakubwa.

Kina baba mliweza, niliposhindwa lolote,
Siku nilizojikaza, mlinifaa kwa yote,
Nawaombea Muweza, baraka nyingi mpate,
Washirika nashukuru, mlinifaa pakubwa.

Vijana nawapongeza, kwa mengi mliyotenda,
Niliona muujiza, ugonjwa nikaushinda,
Yesu ndiye ataweza, kwa baraka kuwalinda,
Washirika nashukuru, mlinifaa pakubwa.

Msaada nilipata, kwenu nilipohitaji,
Fadhila hamkusita, kwa huo wenu upaji,
Mazito nimeyapita, nyote nawavika taji,
Washirika nashukuru, mlinifaa pakubwa.

Maombi yanayo nguvu, tuombalo hujibiwa,
Kujitenga na maovu, kwa Mungu twasikiwa,
Yatakiwa uvumilivu, jambo la maombi huwa,
Washirika nashukuru, mlinifaa pakubwa.

Natamatisha shairi, nimewapa shukurani,
Injili mkihubiri, iwazidie hisani,
Anayetenda mazuri, huyapata ya thamani,
Washirika nashukuru, mlinifaa pakubwa.

© Kimani wa Mbogo

Shairi hili linaelezea shukurani na heshima kwa washirika ambao wamekuwa msaada mkubwa katika maisha ya mtunzi. Hisia za kumshukuru na kuthamini ushirikiano wa washirika zinajitokeza kwa nguvu, huku akitaja changamoto alizokabiliana nazo na namna walivyojitoa bila kuhesabu. Ujumbe wake ni kuonyesha umuhimu wa umoja na msaada wa jamii katika kushinda matatizo, na kuwasihi washirika wote waendelee kuimarisha imani na kusaidiana.

Lengo kuu

Dhamira kuu ya shairi hili ni kutoa shukurani kwa washirika ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha malengo na kushinda matatizo mbalimbali. Mtunzi anaonyesha umuhimu wa ushirikiano na msaada wa kiroho kutoka kwa jamii, kuonyesha kuwa pamoja tunaweza kushinda migumu.

Mandhari

Muktadha wa shairi hilo unajikita katika mazingira ya kijamii na kiroho, ambapo washirika wanachukuliwa kama msingi wa msaada na nguvu. Ni katika jamii ya kiroho ambapo waamini wanashirikiana, wakisaidiana katika maombi na matendo mema, na hivyo kufikia malengo ya kiroho na kijamii.

Wahusika

Wahusika katika shairi hili ni washirika wa kiroho, ikiwemo kina mama, kina baba, na vijana. Kila kundi linaelezwa kuwa na jukumu muhimu katika kumsaidia mtunzi. Kila mmoja anapewa sifa kwa ushirikiano na juhudi zao zilizosaidia katika kumsaidia mtunzi kushinda changamoto.

Hadhira Inayolengwa

Hadhira inayolengwa ni waamini na washirika katika makanisa na jamii zinazoshirikiana kiroho. Shairi linawafikia watu wanaotafuta msaada na ushirikiano katika maisha yao ya kiroho na ya kila siku, kuwatia moyo kuendelea kusaidiana na kushukuru.

Msimamo wa Mtunzi

Mtunzi anaonyesha msimamo wa shukrani na kuthamini kazi nzuri zinazofanywa na washirika wake. Anahimiza umuhimu wa ushirikiano na maombi katika maisha ya kila siku, na kuwasihi waendelee kuimarisha imani yao na kufanya mema katika jamii.

28 1

Maoni ya Wasomaji

Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa.

Andika Maoni

Shiriki mawazo yako kwa heshima. Baruapepe yako haitachapishwa wala kuonekana kwa wasomaji.