Huu ni Utenzi wote wa Mwana Kupona (jumla beti 102) kama ulivyorekodiwa katika maandiko ya fasihi ya Kiswahili. Mashairi yamenukuliwa katika lugha ya Kiswahili asili (lafudhi ya Kipate/Kiamu, mwandiko wa kiutendi) bila tafsiri, ili kumwezesha
Utenzi wa Mwana Kupona
- Negema wangu binti,
mchachefu wa sanati
upulike wasiati
asa ukanzingatia.- Maradhi yamenshika
hatta yametimu mwaka
sikupata kutamka
neno lema kukwambia.- Ndoo mbee ujilisi
na wino na qaratasi
moyoni nina hadithi
nimependa kukwambia.- Ukisa kutaqarabu
Bismillahi kutubu
umsalie Habibu
na sahabaze pamoya.- Ukisa kulitangaza
ina la Mola Muweza
basi tuombe majaza
Mola tatuwafiqia.- Mwanaadamu si kitu
na ulimwengu si wetu
walau hakuna mtu
ambao atasalia.- Mwanangu twaa waadhi
pamoya na yangu radhi
Mngu atakuhifadhi
akuepue na baa.- Twaa nikupe hirizi
uifungeto kwa uzi
uipe na taazizi
upate kuyangalia.- Nikutungie kindani
cha lulu na marijani
nikuvike mke shani
shingoni kikizagaa.- Penda nikupe kifungo
kizuri kisicho ongo
uvae katika shingo
utaona manufaa.- Yangu utakaposhika
mwanangu hutosumbuka
duniani utavuka
na akhira utakia.- La kwanda kamata dini
faradhi usiikhini
na sunna ikimkini
ni wajibu kuitia.- Pili uwe na adabu
na ulimi wa thawabu
uwe mtu mahabubu
kula utakapongia.- La tatu uwe sadiqi
wambiwao ulithiqi
mtu asoshika haqi
sandamane naye ndia.- Tena mwanangu idhili
mbee za maqabaili
uwaonapo mahali
angusa kuwenukia.- Wangiapo wenukie
na moyo ufurahie
kisa uwapeke mbee
watakapokwenda ndia.- Ifanye mteshiteshi
kwa maneno yaso ghashi
wala sifanye ubishi
watu wakakutukia.- Nena nao kwa mzaha
yaweteao furaha
iwapo ya ikraha
kheri kuinyamalia.- Wala situkue dhana
kwa mambo usoyaona
na kwamba na kunong’ona
tahadhari nakwambia.- Sitangane na watumwa
illa mwida wa khuduma
watakuvutia tama
la buda nimekwambia.- Sandamane na wainga
wasoyua kuitunga
ziumbe wasio tanga
wata kuwaqurubia.- Mama pulika maneno
kiumbe ni radhi tano
ndipo apate usono
wa akhera na dunia.- Nda Mngu na Mtumewe
baba na mama wayuwe
na ya tano nda mumewe
mno imekaririwa.- Naawe radhi mumeo
siku zote mkaao
siku mukhitariwao
awe radhi mekuwea.- Na ufapo wewe mbee
radhi yake izengee
wende uitukuzie
ndipo upatapondia.- Siku ufufuliwao
nadhari ni ya mumeo
taulizwa atakao
ndilo takalotendewa.- Kipenda wende peponi
utakwenda dalhini
kinena wende motoni
huna budi utatiwa.- Keti naye kwa adabu
usimtie ghadhabu
akinena simjibu
itahidi kunyamaa.- Enda naye kwa imani
atakalo simkhini
we naye sikindaneni
ukindani huumia.- Kitoka agana naye
kingia mkongowee
kisa umtengezee
mahala pa kupumua.- Kilala siikukuse
mwegeme umpapase
na upepo asikose
mtu wa kumpepea.- Kivikia simwondoe
wala sinene kwa yowe
keti pao siinue
chamka kakuzengea.- Chamka siimuhuli
mwandikie maakuli
na kumtunda mwili
kumsinga na kumwoa.- Mnyoe mpalilize
sharafa umtengeze
na udi umfukize
bukurata wa ashia.- Mtunde kama kijana
asiyoyua kunena
kitu changalie sana
kitokacho na kungia.- Mpumbaze apumbae
amriye sikatae
maovu kieta yeye
Mngu atakulipia.- Mwanangu siwe mkoo
tenda kama uonao
kupea na kosha choo
sidharau mara moya.- Na kowa na kuisinga
na nyee zako kufunga
na asmini kutunga
na firashani kutia.- Nawe ipambe libasi
ukae kama arusi
maguu tia kugesi
na mikononi makoa.- Na kidani na kifungo
sitoe katika shingo
mwili siwate mwingo
kwa marashi na dalia.- Pete sikose zandani
hina sikome nyaani
wanda sitoe matoni
na nshini kuitia.- Nyumba yako i nadhifu
mumeo umsharifu
wakutanapo sufufu
msifu na kumtaya.- Muyuwe alipendalo
nawe ufuate lilo
jambo limtukialo
siwe mwenye kumwedea.- Na ukitaka kutoka
sharuti rukhusa taka
uonapo meudhika
rudi na kuikalia.- Fuata yake idhini
awe radhi kwa yaqini
wala sikae ndiani
saa yake ikasia.- Wala sinene ndiani
sifunue shiraani
mato angalia tini
na uso untie haya.- Rejea upesi kwako
ukae na mume wako
utengeze matandiko
mupate kuilalia.- Mume wako mtukuze
sifa zake zieneze
wala simsharutize
asichoweza kutoa.- Akupacho mpokee
na moyo ufurahie
asolitenda kwa yeye
huna haja kumwambia.- Uonapo uso wake
funua meno uteke
akwambialo lishike
illa kuasi Jalia.- Mama sinue ulimi
nioleza wako umi
nalioa nyaka kumi
tusitete siku moya.- Alinioa babako
kwa furaha na ziteko
tusondoleane mbeko
siku zote twalokaa.- Siku moya tusitete
ovu langu asipate
na lake nisilikute
hatta akakhitariwa.- Yalipokuya faradhi
kanikariria radhi
nkashukuru nkafawidhi
moyo wangu nkatoshea.- Tangu hapo hatta yeo
siyanyamaa kilio
nikumbukapo pumbao
na wingi wa mazoea.- Watu wakipulikana
milele hukumbukana
illa wenye kushindana
daima huiyutia.- Mausio ya mvuli
Allah Allah yaamili
na nduguzo na ahali
wapende nakuusia.- Uwaonapo swahibu
ambao wakunaswibu
wakwambiapo qaribu
angusa kuqurubia.- Na wachandika chakula
uchambiwa nawe nla
wala siweke muhula
nyumanyuma kurejea.- Wala sifanye kiburi
mla hata ushakiri
usiyakuta siqiri
ukamba ni kondolewa.- Watu wote waumini
kwako na wawe wendani
sipende masalatini
washinde ukiwepua.- Sipende wenye jamali
na utukufu wa mali
fuqara ukamdhili
cheo ukamvundia.- Akupendao mpende
akuchezo (akuchukizao) mwenende
kwa zema mvundevunde
laala akiridhia.- Na ayapo muhitaji
mama kwako simuhuji
kwa uwezalo mbuji
angusa kumtendea.- Mama haya yasikize
tafadhali sinipuze
utaona nafuuze
za akhera na dunia.- Tamati maneno yangu
kukuusia mwanangu
sasa ntamuomba Mngu
anipokelee dua.- Kwani yote ninenao
mwanaadamu ni pou
Mola ndiye awezao
kupoteza na kongoa.- Nakuombawe Manani
unitilie auni
ninenayo ulimini
na yote nisoyatoa.- Yote nimezoyanena
Rabbi taqabali minna
na yasalieo tena
Rabbi Mola nitendea.- Niwekea wangu wana
na umbu langu mnuna
yakue yao maina
yenee majimbo pia.- Rabbi waweke nduzangu
na wana wa ndugu zangu
wenee na ulimwengu
kwa jamala na sitawa.- Na jamii islamu
Mola wangu warehemu
matakwa yao yatimu
na nyoyo kufurahia.- Ya Allahu wangu wana
nimekupa ni amana
watunde Mola Rabbana
siwate kuwangalia.- Nimekupa duniani
watunde uwakhizini
unipe kesho peponi
mbee za Tumwa Nabia.- Wangalie kwa huruma
waongoze ndia njema
uwepulie na tama
za akhira na dunia.- Kukuombawe sikomi
wala sifumbi ulimi
ya Mufarrija ’lHammi
nikomeshee udhia.- Nisimeme muhitaji
mjao nakutaraji
alili bi ’l-faraji
ya afua na afia.- Nondolea ndwe mbovu
yaloningia kwa nguvu
dhambi zangu na maovu
ya Rabbi nighufiria.- Kwetu yangawa mazito
kwako wewe ni matoto
nepulia uvukuto
uepuke mara moya.- Nakuombawe Latifa
unondolee makhafa
kwa yaumu ’l-Arafa
na idi ya udhuhia.- Kwa siku hizi tukufu
za kuhiji na kutufu
niafu Rabbi niafu
unishushize afua.- Ya Allahu ya Allahu
ya Rabbahu ya Rabbahu
ya Ghayata Raghbatahu
nitika hukwamkuwa.- Nakuombawe Rabbana
bi asmaika ’l-husna
tisa wa tisiina
mia kupungua moya.- Nipulishie walimu
wakinena yafahamu
dua hini Islamu
akiomba hujibiwa.- Nami mjao dhaifu
mwenye nyingi taklifu
nakuomba takhfifu
Rabbi nitakhafifia.- Nakuomba taisiri
mambo nisoyaqadiri
unegeshe kulla kheri
shari ukinepulia.- Ya Rabbi nitimiliza
mambo nisiyoyaweza
wala moyoni kuwaza
kwamba yatasikilia.- Rabbi unifurahishe
mambo mema unegeshe
maovu uyagurishe
tusikutane pamoya.- Uniweke duniani
miongoni ya wahusuni
nifapo nende peponi
makao ya hafidhiwa.- Ntungile utungo hunu
kwa zehemu na zitunu
kwa qadha yako Dayyanu
na hukumuzo Jalia.- Ntungile nili saqimu
moyo usina fahamu
usomeni Islamu
mukiogozana ndia.- Na sababu ya kutunga
si shairi si malenga
nina kijana muinga
napenda kumuusia.- Napenda kumnabihi
laala katanabahi
kamfuata illahi
pamwe na wake rijaa.- Somani nyuate huramu
maana muyafahamu
musitukue laumu
mbee za Mola Jalia.- Somani mite ya nganu
mutii waume wenu
musipatwe na zitunu
za akhera na dunia.- Mwenye kutii mvuli
ndaka jaha na jamali
kula endapo mahali
hutangaa yake ndia.- Mwenye kutunga nudhumu
ni gharibu mwenye hamu
na ubora wa ithimu
Rabbi tamghufiria.- Ina lake mufahamu
ni mtaraji Karimu
Mwana Kupona Mshamu
Pate alikozaliwa.- Tarikhiye kwa yaqini
ni alifu wa miyateni
khamsa wa sabiini
hizi zote hijiria.- Na baitize idadi
ni miati maadudi
na mbili za mazidadi
ndizo zimezozidia.- Mola tatusahilia
kwa baraka za Nabia
na masahaba pamoya
dini waliotetea.- Nahimidi nkisalia
kwa Tume wetu Nabia
ali zake na dhuria
itwenee sote pia.
(Asili: Mashairi haya yamenukuliwa kutoka miswada ya asili ya utenzi yaliyochapishwa katika kitabu “Tendi: Traditional Swahili Poems” kilichohaririwa na J. W. T. Allen, 1971.)
193
3
Maoni ya Wasomaji
Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa.
Andika Maoni
Shiriki mawazo yako kwa heshima. Baruapepe yako haitachapishwa wala kuonekana kwa wasomaji.