Sabilia Katika Ushairi wa Kiswahili

Tarehe: Machi 21, 2025 - Kimani wa Mbogo

Sabilia ni aina ya shairi la Kiswahili lenye sifa ya kutokuwa na kibwagizo. Tofauti na mashairi ya kimapokeo yanayorudia mshororo wa mwisho (kama kibwagizo), shairi la sabilia halirudii mstari wowote wa mwisho, bali kila ubeti huwa na kituo cha mwisho kinachojitegemea.

Neno sabilia linahusiana na kitenzi kusabilia, ambacho humaanisha kumwachia mtu uhuru wa kuchagua au kufanya atakavyo. Hali hii inaakisiwa katika muundo wa shairi la sabilia, ambapo mshairi hana wajibu wa kurudia kituo maalum, bali hujenga kila ubeti kwa uhuru wake wa kisanaa.

Sifa za Sabilia

  • Hakuna kibwagizo kinachorudiwa kutoka ubeti mmoja hadi mwingine
  • Kituo cha mwisho wa kila ubeti hujitegemea, kikitoa maana kamili
  • Huonyesha uhuru wa mtunzi katika kuhitimisha kila ubeti kwa namna ya kipekee
  • Hufuata mtiririko wa kimawazo, bila kuvunjwa na kurudia mstari
  • Hutoa fursa ya kusisitiza mawazo mbalimbali katika kila ubeti

Mfano wa Sabilia – Kimani wa Mbogo

Hutonipata makazi, nyumbani napumzika
Japo ninao ujuzi, mapeni yametoweka
Mifuko ina uwazi, sina pa kufurahika
Ninavyoifanza kazi, ninazidi kuteseka

Nimebaki nikiwaza, kila kutwa nateseka
Kujimudu sijaweza, hifadhi nikaiweka
Mbele yangu kuna kiza, sijui nitavyovuka
Kila ninapojikaza, moyo wangu navunjika

~ Kimani wa Mbogo

Ufafanuzi wa Mfano

Kila ubeti una mishororo minne, lakini kibwagizo (mstari wa mwisho) wa kila ubeti ni tofauti, yaani:

  • Ubeti wa kwanza: “Ninavyoifanza kazi, ninazidi kuteseka”
  • Ubeti wa pili: “Kila ninapojikaza, moyo wangu navunjika”

Hakuna kurudiwa kwa mstari wowote wa mwisho — na kila ubeti unajitegemea kimaana. Hii ndiyo sifa kuu ya sabilia.

Umuhimu wa Sabilia Katika Fasihi ya Kiswahili

  • Huonyesha uhuru wa kifasihi kwa mshairi kuchagua mwelekeo wa kila ubeti
  • Huongeza utofauti wa maudhui kwa kila ubeti kuwa na msisitizo wake binafsi
  • Hufanikisha uwasilishaji wa hisia au hali kwa namna pana zaidi
  • Huongeza ubunifu, kwa kuwa mshairi anahitaji kutunga kila ubeti kwa nguvu ya maana mpya
164 0

Maoni ya Wasomaji

Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa.

Andika Maoni

Shiriki mawazo yako kwa heshima. Baruapepe yako haitachapishwa wala kuonekana kwa wasomaji.