Panda Miti
Tathnia • Mazingira • Waadhi

Panda Miti

Tarehe: Januari 1, 2005 - Kimani wa Mbogo

Panda Miti

Tupande mbuni, tupate, kahawa kinywani,
Kwa mdalasini, tupate, kiungo mloni.

Mkaajabali, tupate, dawa ya machoni,
Kwa mshelisheli, tupate, tunda chemsheni.

Tupande mkanya, tupate, dawa mauani,
Na kwa mvungunya, tupate, mandhari mitini.

Tupande mtonga, tupate, matunda vinywani,
Kwa mkomamanga, tupate, kwendesha fungeni.

Tupande mng'ongo, tupate, dawa kifuani,
Kwa mkatafungo, tupate, kamba magomeni.

Tupande mtini, tupate, toka kwake tini,
Kwa mdoriani, tupate, zake doriani.

Tupande mbuyu, tupate, ladha chakulani,
Tupande mkuyu, tupate, diro aridhini.

Tupande mkwara, tupate, fimbo pia kuni,
Na kwa mkwakwara, tupate, mboga kwa majani.

Tupande mpesi, tupate, nguvu mishipani,
Mkoniferasi, tupate, kurasa mbaoni.

Panda mkamasi,, tupate, mlo telezini,
Na kwa mkakasi, tupate, urefu laini.

Kwa mkarafuu, tupate, kiungo mloni,
Kwa mkunatuu, tupate, dawa ya jandoni.

Panda mbingiri, tupate, kutapishiani,
Kwa msonobari, tupate, majano mbaoni.

Tupande mkoko, tupate, dawa ya ngozini,
Na kwa mtomoko, tupate, tomoko kondeni.

Tupande mkumbi, tupate, kili kupikeni,
Na kwa mbirimbi, tupate, ladha acharini.

Tupande mkaa, tupate, dawa kohozini,
Na kwa mkandaa, tupate, rangi kofiani.

Panda mtumbati, tupate, ugumu mbaoni,
Kwa msanapiti, tupate, nakishi uani.

Tupande mkoronge, tupate, ua mijengoni,
Tupande mkenge, tupate, vivuli mijini.

Panda mkunazi, tupate, kunazi vinywani,
Na kwa mbaazi, tupate, mbegu vitumboni.

© Kimani wa Mbogo

Shairi hili ni wimbo wa kuhamasisha jamii kuhusu kupanda miti ya aina mbalimbali kwa manufaa ya chakula, tiba, kivuli na urembo wa mazingira. Mtunzi anaorodhesha miti kwa mtindo wa kishairi, akieleza faida za kila mti unaopandwa.

Shairi linaonesha kwamba miti si tu mapambo ya asili, bali ni chanzo kikuu cha lishe, tiba, ustawi wa mazingira, na maisha bora. Kupanda miti ni kujenga afya, uchumi na uzuri wa maisha ya kila siku.

Lengo kuu

Lengo la mtunzi ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira kupitia upandaji wa miti yenye manufaa. Anataka jamii ione thamani ya miti kama sehemu ya suluhisho la changamoto za kiafya, kijamii na kiuchumi.

Mandhari

Mandhari ya shairi ni kijiji au jamii ya kawaida ambapo watu wanaweza kulima na kupanda miti karibu na makazi yao, mashambani, au maeneo ya umma.

Wahusika

Wahusika wakuu ni watu wa jamii—wanaohimizwa kupanda miti, na miti yenyewe ambayo inatajwa kwa majina na faida zake. Mtunzi anajitokeza kama mtoa elimu na mwaliko wa matumaini.

Hadhira Inayolengwa

Shairi linaelekezwa kwa watu wote, hasa wakulima, wanafunzi, viongozi wa jamii, na watunzaji wa mazingira. Pia linawafaa watoto kwa elimu ya asili.

Msimamo wa Mtunzi

Mtunzi ana msimamo wa kiikolojia na kijamii, akiamini kuwa upandaji wa miti ni kitendo cha hekima, afya, na maendeleo endelevu. Anatilia mkazo urithi wa asili na matumizi ya miti kama sehemu ya maisha bora.

12 0

Maoni ya Wasomaji

Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa.

Andika Maoni

Shiriki mawazo yako kwa heshima. Baruapepe yako haitachapishwa wala kuonekana kwa wasomaji.

Ingia kwa Google ili kutoa maoni kwa jina lako.

Endelea kwa Google