Mcheka Kilema
Ukaraguni • Hekima • Methali

Mcheka Kilema

Tarehe: Januari 1, 2005 - Kimani wa Mbogo

Mcheka Kilema

Silika yangu wacheka, hunioni mahashumu,
Ufyonzi watukutika, yote kwa kutaamamu,
Wanitundika mahoka, nisiye nazo timamu,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Sikani kwa udhilifu, upungufu wa akili,
Busara yangu dhaifu, legevu yangu tamuli,
Matendo ya ukashifu, ni kwa hii yangu hali,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Nyota kutano kichwano, taka za kipilipili,
Vazi upurukushani, laonyesha yangu hali,
Uchafuko kusakini, abadi kwa azali,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Kutwaa taka sokoni, na fumba kuibebea,
Uhaji ni upindani, shabuko lakuotea,
Shambulio ni usani litendalo kunyendea,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Wanicheka unadhifu, kutenga wangu urari,
Wauona ukashifu, ubashiri kuhadhiri,
Wanicheka uvunjifu, wajiona kushamiri,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Kutuzi ni shambulio, ulio wa ufukuto,
Mwakumbatia kimbio, la kuume kwa kushoto,
Ganjo lao kimbilio, vinionapo vitoto,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Kila mara mwalipuka, vishindo vya kishetani,
Uhali wangu mwacheka, udadisi wa utani,
Pale pole napozuka, nawapata wapindani,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Ni leo ti mwanicheka, keshoi wenu waumbuka,
Kesho yenu ni uzuka, licha ya kuvivinyuka,
Kichaa nacho ukoka, kitambacho kwa hakika,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

Huo wenu ni upofu, hatimaye usoona,
Enyi ndio wapunjufu, walio na uhiana,
Wana wa uharibifu, na wema mkijiona,
Anayecheka kilema, hafi bila kumfika.

© Kimani wa Mbogo

Shairi hili ni tamko la maumivu na ujasiri kutoka kwa mtu anayeishi na hali ya ulemavu au changamoto fulani, huku akikumbana na dhihaka, kejeli, na dharau kutoka kwa jamii. Mtunzi anatoa onyo lenye busara: “Anayecheka kilema, hafi bila kumfika” – akimaanisha kwamba dharau na kebehi si salama kwa yeyote, kwani maisha hubadilika.

Ujumbe mkuu ni kwamba kudharau au kucheka mtu mwenye ulemavu au changamoto ni ukosefu wa utu na hekima. Mtunzi anakemea tabia ya kebehi kwa watu waliopo kwenye hali ngumu, akisisitiza kuwa kila mtu yuko kwenye mzunguko wa maisha, na majaribu yanaweza kumkumba yeyote. Ulemavu si sababu ya dharau, bali ni sababu ya huruma na heshima.

Lengo kuu

Lengo ni kuelimisha jamii kuheshimu na kuwathamini watu wenye ulemavu au waliopo katika mazingira magumu. Pia ni kutia moyo wale wanaochekwa au kudhalilishwa, kuwa wanyenyekevu lakini thabiti, kwani siku moja mabadiliko huja.

Mandhari

Mandhari ya shairi ni ya kijamii na kihisia, ambapo kuna mkutano wa maisha ya mnyonge na macho ya kejeli ya waliomzunguka. Picha za mitaani, mavazi, taka, na hali ya kifukara zinatumika kueleza hali ya udhalilifu anayoishi nayo mhusika.

Hadhira Inayolengwa

Shairi linaelekezwa kwa jamii nzima, hususan watu wenye tabia ya kukejeli, kudharau au kuwabeza wengine kwa mwonekano wao wa nje. Pia linawahimiza watu waliodhalilishwa wawe na subira na kujiamini.

Msimamo wa Mtunzi

Mtunzi ana msimamo wa kulinda heshima ya binadamu, bila kujali hali yake ya nje. Anapinga vikali ukatili wa maneno na dharau kwa watu walio na ulemavu au changamoto. Msimamo wake unaonyesha kuwa hakuna aliye salama na mzunguko wa maisha, na kwamba kiburi cha leo kinaweza kuwa fedheha ya kesho.

18 0

Maoni ya Wasomaji

Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa.

Andika Maoni

Shiriki mawazo yako kwa heshima. Baruapepe yako haitachapishwa wala kuonekana kwa wasomaji.

Ingia kwa Google ili kutoa maoni kwa jina lako.

Endelea kwa Google