Masingizio Siyataki
Ya nyumbani na ya siri, hao wanakupa yani?
Na wasema ni dosari, mambo yangu ya kanuni,
Nao hao wafikiri, yatamfaidi nani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.Wasikiza wadadisi, na kunipuza kwa nini?
Kumbe hao wajasusi, kwa kweli ni wafitini,
Habari za wafilisi, sikio watega lani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.Njiani we wanipita, na vidomo kimya kwani?
Kuongea unakata, ati hutaki uneni,
Kufanya mambo kutata, ndiko kuwa ufanani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.Wasema nimekufuru, wanidhulumia nini?
Uniache niwe huru, siutaki ubishani,
Na kamwe usinizuru, utanizuru kwa nini?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.Matendo kanuni yangu, yanakusakama kwani?
Tumekuwa nao kwangu, takwimu nyingi nyumbani,
Kuwakosoa wanangu, waniulizia yani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.Kosa ni langu wasema, nimemkosea nani?
Na ikiwa ni Karima, basi sio kanisani,
Kwa mwana nitubu hima, yakini mzazi nani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.Maneno kwa kusanjari, waniingilia kwani?
Usinitakie shari, kwa Mola ni barakani,
Waniambia nikiri, dhambi wapi walakini?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.Leo waniangazia, kosa kalipata lini?
Ila wanitafutia, wabagua yangu sini,
Yote kwa kupindukia, ubaguzi nao wani?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.Sababu dinari sina, ndio maana utani?
Kwa madhahabu naona, dinari ndiyo hisani,
Wale dinari hawana, hawatapasi langoni?
Unapoamua jambo, yafaa ulitafiti.
Shairi hili linaeleza hali ya mtu anayeshutumiwa au kuhukumiwa na jamii bila sababu ya msingi. Mshairi anaonyesha jinsi watu wanavyoingilia maisha yake, kumchunguza, na hata kumhukumu bila haki, lakini anasisitiza kuwa kabla ya kufanya maamuzi au kutoa hukumu, watu wanapaswa kufanya utafiti wa kina.
Shairi linaeleza kwamba kabla ya mtu kuamua au kuhukumu jambo, ni muhimu kulitafiti kwa kina. Linaonya dhidi ya tabia ya kuingilia mambo ya wengine, kusambaza habari za uongo, au kubagua kwa misingi ya mali, hadhi au chuki binafsi.
Lengo kuu
Lengo ni kupinga ukosefu wa haki na uzushi, pamoja na kulinda haki ya mtu binafsi kufanya maamuzi au kuishi bila kuingiliwa kwa mabaya. Pia ni mwito wa jamii kuwa na hekima, subira na busara kabla ya kutoa hukumu kwa wengine.
Mandhari
Mandhari ya shairi ni kijamii na binafsi, likionyesha hali ya mtu anayeonewa, anayetengwa au anayezushiwa mambo yasiyo ya kweli, huku jamii ikimkosoa kwa upendeleo au kwa upotoshaji.
Hadhira Inayolengwa
Shairi linaelekezwa kwa watu wa kawaida, viongozi wa kijamii, na jamii kwa ujumla—likiwa wito wa kujitathmini, kuacha kuingilia mambo yasiyowahusu, na kuwa waangalifu kabla ya kuhukumu au kueneza habari.
Msimamo wa Mtunzi
Mtunzi ana msimamo wa kutetea haki ya mtu binafsi, kupinga unafiki na kutaka jamii iwe ya haki na ya kweli. Anapinga tabia ya kukosoa au kuingilia wengine kwa kisingizio cha “kanuni” au “imani,” bila kuelewa kiini cha mambo.
Maoni ya Wasomaji
Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa.
Andika Maoni
Shiriki mawazo yako kwa heshima. Baruapepe yako haitachapishwa wala kuonekana kwa wasomaji.
Ingia kwa Google ili kutoa maoni kwa jina lako.