Kuhama Kitongoji
Ukaraguni • Maisha

Kuhama Kitongoji

Tarehe: Januari 1, 2004 - Kimani wa Mbogo

Kuhama Kitongoji

Nisaidie Karima, kutenda yalio mema,
Nataka niweze hama, hiki kijiji kwa hima,
Kijiji cha wanachama, wa matendo yaso mema,
Kitongojini kulima, dhambi na yasiyo mema.

Mtu aliyezaliwa, kwa Mola hubarikiwa,
Hupewa chake kipawa, kujilinda kwa ukiwa,
Mwadilifu kugusiwa, asiweze sawasawa,
Abaki yu ufidiwa, baraka zake akawa.

Kutunukiwa hedaya, niipate bila haya,
Zisimuliwe hekaya, Masihi yake himaya,
Kuipata si vibaya, na kuwa nacho kinaya,
Kupewa naye Mesaya, kutoka kwa yake himaya.

Natazama kijijini, wimbo huu kuughani,
Ni mengi yalio ndani, na wengi kitongojini,
Waasi wenye uhuni, kafungiwa kwa husuni,
Watundu na wakunguni, furaha yao ugoni.

Hakika hiki kijiji, ni wengi wanaohama,
Wao mie nawahoji, kwa nini wao hawaji,
Hujitokeza kwa jiji, wao kuwa na ujaji,
Hao wanakitongoji, fanaka hawataraji.

Ufanisi unikifu, kwako uwe utukufu,
Baraka zije kwa safu, moyo uwe mkujufu,
Kwa mambo ya uraufu, yasiwe uharibifu,
Yasiwe na upungufu, daima nisije hofu.

© Kimani wa Mbogo

Shairi hili ni sala na ombi la mtu anayetaka kuondoka katika kijiji kilichojaa maovu, akimwomba Karima (Mwenyezi Mungu) msaada ili aishi maisha ya mema, yaliyojaa baraka, hekima na uadilifu. Ni shairi la toba, tafakari na tamaa ya mabadiliko.

Shairi linaeleza tamaa ya kujitenga na mazingira ya dhambi na kuishi maisha ya haki, maadili na baraka za kiroho. Mtunzi anahoji hali ya kijiji kilichojaa waasi, wazinzi na wahuni, na kutamani hama kwa ajili ya ufanisi na utukufu wa Mungu.

Lengo kuu

Lengo ni kuhimiza kujitathmini kimaadili na kujitenga na uovu, pia linaonyesha umuhimu wa kumtegemea Mungu kwa msaada wa kufikia maisha bora na yaliyo sahihi kiroho.

Mandhari

Mandhari ya shairi ni ya kijamii na kiroho, likifanyika kijijini—mahali palipojaa watu wenye tabia potovu, ambapo mtunzi anajitahidi kutafuta njia ya kuondoka na kupata wokovu.

Hadhira Inayolengwa

Shairi linaelekezwa kwa watu wote wanaotamani mabadiliko ya maisha, hasa wale waliokata tamaa au wanaoishi katika mazingira magumu ya kimaadili.

Msimamo wa Mtunzi

Mtunzi ana msimamo wa kutafuta utakatifu, baraka na kujitenga na uovu, akiwa na matumaini kuwa kwa msaada wa Mungu ataondoka kwenye mazingira mabaya na kuishi maisha ya mema, yenye hofu ya Mungu na mafanikio ya kweli.

14 0

Maoni ya Wasomaji

Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa.

Andika Maoni

Shiriki mawazo yako kwa heshima. Baruapepe yako haitachapishwa wala kuonekana kwa wasomaji.

Ingia kwa Google ili kutoa maoni kwa jina lako.

Endelea kwa Google