Heri Njema Iwe Kwako
Ukaraguni • Hekima

Heri Njema Iwe Kwako

Tarehe: Januari 1, 2005 - Kimani wa Mbogo

Heri Njema Iwe Kwako

Sikiliza nakwambia, ewe bwana mdubiri,
Ulo karibu fifia, nisikize tafadhari,
Lile utalosikia, liige ulikithiri,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Wajiona na upweke, raha maishani huna,
Weye wajiona peke, sudi njema nayo huna,
Hili wazo uepuke, tegemea Mola Bwana,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Mkata kinyongo hana, cha nini wajiwekea?
Bahati wasema huna, ukata wanyenyekea,
Hohehehe wajiona, bahati utapokea,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Ufukara wauona, na kujipuza kwa nini?
Kiatu wasema huna, cha kuvaa mguuni,
Mwengine mguu hana, yeye atasema nini?
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Unasema ni laana, mganga waenda kwake,
Warudi huku wanuna, ni kali shauri lake,
Mbuzi wa manjano huna, wa kumpeleka kwake,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Yohana kumi na nne, hapo sita Biblia,
Uisome kwa makine, Bwana Yesu ndiye njia,
Huu ugonjwa upone, jaribu kumtegemea,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Mwenyezi tunfuate,tuyatende yalo mema,
Nazo baraka tupate, kutoka kwake Karima,
Nakwambia yafuate, uupate usalama,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Siku moja itafika, mdubira bahatini,
Naye paka atasaka, panya nje pia ndani,
Yule paka kuteseka,naye bila bahatini,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

© Kimani wa Mbogo

Shairi hili ni wito wa matumaini, toba, na mwelekeo wa kiroho kwa mtu anayejiona mnyonge au aliyekata tamaa maishani. Mtunzi anamfariji na kumwelekeza kwa Mungu kama chanzo cha faraja na tumaini.

Ujumbe ni kwamba kila mtu ana nafasi ya mabadiliko, hata akihisi hana thamani au bahati. Heri njema itakuja iwapo atamtegemea Mungu kwa moyo wa unyenyekevu.

Lengo kuu

Lengo ni kumtia moyo mtu aliyevunjika moyo, kumwelekeza kwa imani na kuondoa mawazo ya kukata tamaa au kujionea huruma kupita kiasi.

Mandhari

Mandhari ya shairi ni ya kiroho na kijamii, inayomgusa mtu wa hali ya chini, aliye katika upweke, ufukara, au changamoto za maisha.

Wahusika

Mhusika mkuu ni mtu anayekata tamaa, na mtunzi anamzungumzia moja kwa moja. Mungu pia ni mhusika wa kimya anayependekezwa kama msaada wa kweli.

Hadhira Inayolengwa

Shairi linaelekezwa kwa watu wote waliopoteza tumaini au waliovunjika moyo, hasa wale wanaojiona wamesahaulika au waliopuuzwa na jamii.

Msimamo wa Mtunzi

Mtunzi ana msimamo wa matumaini, imani kwa Mungu, na huruma kwa wale waliokata tamaa. Anaamini kuwa kila mtu anaweza kubadilika na kupata heri.

11 0

Maoni ya Wasomaji

Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa.

Andika Maoni

Shiriki mawazo yako kwa heshima. Baruapepe yako haitachapishwa wala kuonekana kwa wasomaji.

Ingia kwa Google ili kutoa maoni kwa jina lako.

Endelea kwa Google