Ashiki Wakati Usiofaa
Natuone ndipo twambe, kusikia si kuona,
Hili silo la uimbe, ukweli nimeuona,
Nitunga niliimbe, asilani lisofana,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.Kasisi anasikika, neno katupakulia,
Palupiti azunguka, itikadi kututia,
Kasula kajipachika, Masihi kuhimidia,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.Nyie kweli mwatamani, wala hamuwezi pata,
Kuomba mnaombeni, jibu hamjalipata,
Hamuombi kwa makini, ndo mwakawia kupata,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.Ibada kawa nadhifu, kwao walio makini,
Kwangu ilikuwa hofu, baina yao wendani,
Waumini wakisifu, wahibu hawabaini,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.Siti amejikwatua, usoni amemeteka,
Ghulamu jicho angua, mara anapokumbuka,
Haya yote kugundua, nikawa nafedheheka,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.Ishara kwa kusanjari, usoridhisha wakati,
Msukosuko tayari, nilekuwa katikati,
Visura na yao siri, ghulamu na wake siti,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.Kwangu mie nikajuta, kati ya wenzi wendani,
Kikingio wakapata, kaumu kuwa makini,
Langu ni kujikunyata, kama niko mvuani,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.Kwanza sujudu Kahari, baadaye ni mengine,
Haya tena yasijiri, hayo tena tusione,
Ishara kwa kusanjari, ibadani na kwengine,
Ashiki isiyofana, wasaa usiofaa.
Shairi hili linaelezea hali ya kutozingatia ibada kwa baadhi ya waumini, ambapo badala ya kujikita katika kiroho, wanashughulika na mambo ya kimwili au matamanio ya kidunia. Mtunzi analalamikia hali hiyo akihisi fedheha, akieleza kuwa ashiki (tamaa) iliyoonekana haikufaa kwa wasaa (wakati) wa ibada.
Shairi linaonya dhidi ya kuchanganya matamanio ya mwili na mambo ya kiroho, hasa katika mazingira ya ibada. Mtunzi anasisitiza kuwa ibada ni wakati wa utulivu, tafakari na unyenyekevu kwa Mungu, si fursa ya kuonyesha uzuri au kushabikia urembo wa wengine. Ukweli wa kuona hutofautiana na kusikia, na sasa ameona kwa macho, hali isiyofaa.
Lengo kuu
Lengo ni kuamsha dhamira ya waumini kuhusu namna wanavyohudhuria na kushiriki ibada. Mtunzi anapendekeza kuwa watu wajitakase kifikra na kimoyo wanapomwendea Mungu, wasichafue wasaa mtakatifu kwa matendo au mitazamo isiyofaa.
Mandhari
Mandhari ya shairi ni kanisani, wakati wa ibada, ambapo kasisi anaongoza, waumini wanaimba na kusujudu, lakini baadhi yao wamepoteza mwelekeo kwa kuzingatia vitu vya nje kama mavazi, urembo na mitazamo ya kimwili.
Hadhira Inayolengwa
Shairi linaelekezwa kwa waumini wa dini, hasa wale waumini waaminifu lakini wanaoathiriwa na tabia za wengine kanisani. Pia linawahimiza viongozi wa dini na jamii kushughulikia mienendo isiyofaa kwenye maeneo ya ibada.
Msimamo wa Mtunzi
Mtunzi ana msimamo wa uadilifu wa kiroho na heshima kwa ibada. Anaamini kuwa ibada ni tukio takatifu lisilopaswa kuchafuliwa na hisia za ashiki au mivuto ya kimwili. Anaonyesha majonzi, aibu, na majuto kuwa sehemu ya mazingira ambayo hayakufaa kiibada.
Maoni ya Wasomaji
Bado hakuna maoni yaliyoidhinishwa.
Andika Maoni
Shiriki mawazo yako kwa heshima. Baruapepe yako haitachapishwa wala kuonekana kwa wasomaji.
Ingia kwa Google ili kutoa maoni kwa jina lako.