Binadamu Ng’amba

Binadamu kweli ng’ámba, hatakosa la kuamba.
Kutwa kucha atalumba, na tetesi kuziimba.
Hata ‘funge kwa makamba, au limi ukavimba.
Atazidi kujitamba, hatakosa la kuamba.

Mwili wako kijipamba, atasema wajigamba.
Akiketi kwenye chemba, waziwazi takuchimba.
Tapitisha kama bomba, yakafika kwenye vyumba.
Binadamu kama ng’amba, hatakosa la kuamba.

Mato yako ukifumba, kisogocho ataramba.
Ukienda kisambamba, atasema una mimba.
Abadani hatoumba, ada yake nikuchimba.
Binadamu kama ng’amba, hatakosa la kuamba.

Talalama kama samba, akisema u mshamba.
Mola wako ukiomba, bila shaka hutoyumba.
Matetesi akiimba, mambo yako yatatamba.
Binadamu kama ng’amba, hatakosa la kuamba.

Nashukuru na Muumba, Kweni mimi meniumba.
Sifa zake nitaimba, sitojali wakiamba.
Nitazidi kujipamba, hata waja kinichimba.
Binadamu kweli, ng’amba hatakosa la kuamba.

Tamatini na muomba, mkomee kuniimba.
Mimi sio gumbagumba, au mjalo mwembamba.
Mkiona nimepumba, msidhani mimi gumba,
Binadamu kweli ng’amba, hatakosa la kuamba.

©  Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!