Nakubali nimekosa, kuvunda wako mtima
Pembeni nilikutosa, yakuchukiza kasema
Kukataa yako posa, mrututu nikatema
Unisamehe swahibu, kisasi hakifaidi
Tutafakari ya sasa, wazia ya kale mema
Kwa nini unanitesa? ukumbuke wangu wema
Chembeni umenigusa, donda hili laniuma
Unisamehe swahibu, kisasi hakifaidi
Ewe mwenye kutakasa, mpe mwepesi mtima
Yafute yangu makosa, vilio kwako natuma
Sitorudia kukosa, faima sitomfuma
Unisamehe swahibu, kisasi hakifaidi
© Nyangara Mayieka