Shufaa

Nashukuru kwa kusema, asante Mola Karimu
Kwa ulivyonipa ne’ma, leo nashika kalamu
Ni nyongeza ya heshima, mbele ya binaadamu
Nafurahi ni timamu, mimi kupata shufaa

Mimi kupata shufaa, nafurahi ni timamu
Umenipa ushujaa, hapo awali adimu
Na sasa mimi kifaa, watambue maharimu
Nafurahi ni timamu, mimi kupata shufaa

Mola wangu mtukuka, asante kunikirimu
Pembeni sitokuweka, hilo kwangu ni vigumu
Ulonipa nimeshika, hamadi yangu adhimu
Nafurahi ni timamu, mimi kupata shufaa

Umenipa kwa hekima, mtihani umetimu
Nami kwako nainama, amri ninasalimu
Kissamvu kwa taadhima, shukurani zipo humu
Nafurahi ni timamu, mimi kupata shufaa

Mikongolo na Msamvu, ndugu zangu mfahamu
Mimi tena sina gwamvu, bado nipate ghulamu
Huku nasubiri pamvu, uhai ujapodumu
Nafurahi ni timamu, mimi kupata shufaa

Mola wangu niongoze, niitunze na idumu
Katu nisiipoteze, nikaiacha sehemu
Nafahamu uijaze, inifate yangu damu
Nafurahi ni timamu, mimi kupata shufaa

Ilinde kwa halaiki, uijalie nidhamu
Kila palipo handaki, uiepushie zamu
Ailengae fataki, umlipue kwa bomu
Nafurahi ni timamu, mimi kupata shufaa

Kaditama nimefika, japo situpi kalamu
Hakika naliwazika, kwa liwazo maalumu
Kama lingegawanyika, ningelikata kasamu
Nafurahi ni timamu, mimi kupata shufaa

© Hamisi A.S. Kissamvu
Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!