Wangu Pasta

Utetesi sitasita, kuhusu wa kwetu pasta,
Vizuri metukamata, tumefika kwa ukuta,
Wakristu amenata, wamebaki wamesota,
Eneza neno pasta, uwongo wewe wata.

Kanisani twakukuta, ukiwa umetunata,
Mahubiri ya yaso tata, na maneno yaso tata,
Injilini twajikita, mambo mawi kusokota,
Eneza neno pasta, uwongo wewe wata.

Pesa tunazozipata, ni vigumu kuzipata,
Maisha yanatusuta, kama mawe twayagota,
Huna haja kupakata,makondoo tutasita,
Eneza neno pasta, uwongo wewe wata.

Swadaka unaipata, ule bila ya kujuta,
Waniahidi kupata,ukiniita wako sista,
Hela zangu kuambata, kwako wende kula bata,
Eneza neno pasta, uwongo wewe wata.

Miujizani mejikita, umaskini kukata,
Ndipo kweli kuikuta, nikutoa bila tata,
Bwana Yesu hakupata, mbona una utata,
Eneza neno pasta, uwongo wewe wata.

Malenga sijatokota, wala sijawapiga vita,
Ni wazo limenikuta, kuhusu wangu pasta,
Pesa zangu atapata, maendeleo n’tayapata?
Eneza neno pasta, uwongo wewe wata.

© Kiambi Daniel
Mombasa Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!