Mtafutaji Sichoki

Kutwa ninatangatanga, kuitafuta ridhiki
Senti nazichangachanga, japo nipunguze dhiki
Sio wa kumangamanga, vya kupewa siridhiki
Mtafutaji sichoki, kote kote hadi Tanga.

Shida kunizongazonga, kuniumiza sitaki
Mawe nayagongagonga, nipate ya mishikaki
Senti nazikongakonga, ukata sinishtaki
Mtafutaji sichoki, kote kote hadi Tanga.

Siwezi kuangaanga, pasi jasho nimiliki
Mwisho kunihangahanga, vya wenyewe haviliki
Zangu nazipangapanga, zitoshazo kwa iliki
Mtafutaji sichoki, kote kote hadi Tanga.

Sina za kuhongahonga, katukatu sidiriki
Japo wanizongazonga, kwa hili sishauriki
Mengi yanisongasonga, dondoo sitashiriki
Mtafutaji sichoki, kote kote hadi Tanga.

© Evock Miwaga

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!