Elimu na Manufaa

Ninasimama ni wima, nikuli toka moyoni,
Leo mie ninasema, mnisikie Jamani,
Inna jambo akrama, la muhimu aushini,
Elimu na manufaa!

Kuanzia chekechea, neno elimu si geni,
Mengi tumeyasikia, pia siku za usoni,
Bila elimu sikia, tama maisha adhani,
Elimu na manufaa!

Mabinti na auladi, nalingana hadharani,
Suluhu si kama jadi, ukubali dawamuni,
Natusome kwa juhudi, twishi vyema maishani,
Elimu na manufaa!

Elimu ninakwambiya, mipango yake kifani,
Kioo katika kaya, kwake mema abadani,
Na ufikapo ashiya, kuwa mfano yakini,
Elimu na manufaa!

Elimu huheshimiwa, majina mema mwishoni,
Profesa hupatiwa, daktari hutamani,
Waja huwa waswifiwa, elimu wakibaini,
Elimu na manufaa!

Kupatiwa uongozi, cheo chochote fulani,
Bila elimu huwezi, hakuna kukuthamini,
Hata kama ni mbawazi, wewe utaongozani?
Elimu na manufaa!

Walimu na wahadhiri, inna kwenu shukrani,
Uamilifu mzuri, kufanya watu thamani,
Rabana awape heri, na afya njema kazini,
Elimu na manufaa!

Abu na mama kongole, kunikirimu hisani,
Kufanya chochote kile, kulipa karo shuleni,
Hekima tunayo tele, itufae maishani,
Elimu na na manufaa!

© Bett Vincent

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!