Huba la Kweli Likitoka

Ruhusa yenu naomba, yote niyaweke wazi,
Mja nadai kuimba, mnielewe waziwazi,
Rohoni kama mgomba, tulishike bila kazi,
Huba la kweli hakika, likitoka limeenda.

Mapenzi si katu jino, yangolewa na kumea,
Ukipenda mtu mno, mtaishi kama mimea,
Kwani mwili bila kiuno, hayawezi jishikilia,
Huba la kweli hakika, likitoka limeenda.

Ukipenda mtu kweli, kiondoka utalia,
Kwa uzito wa jabali, utashindwa vumilia,
Roho mepata ajali, majonzi yamesalia,
Huba la kweli hakika, likitoka limeenda.

Mapenzi ya kweli kwetu, halina uwingi katu,
Ni sawana na viatu, yavaliwa mbili kwa mtu,
Wako wema sepetu, umpende mbele ya watu,
Huba la kweli hakika, likitoka limeenda.

Andiko matakatifu, yasema upendo kweli,
Mapenzi yetu kwa wafu, walohai wastahili,
Ya ndugu siwe hafifu, ikiwa ya mungu kweli,
Huba la kweli hakika, likitoka limeenda.

Utamu wa penzi dhahiri, kupenda si haiba,
Walopenda kimahiri, wanaitwa wao baba,
Familia utajiri, walikijaza kibaba,
Huba la kweli hakika, likitoka limeenda.

Kibinafsi naketi, penzi ya pesa sipendi,
Rohoni Nina bahati, napendwa pasi wikendi,
Tatengeneza kamati, twasubiri mitabendi,
Huba la kweli hakika, likitoka limeenda.

Niruhusu tamatishe, masikio yasikie,
Penzi letu lisiishe, moyoni tuvumilie,
Wenye ndoa tuwapishe, mapenzi wafurahie,
Huba la kweli hakika, likitoka limeenda.

© Koffi Brian

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!