Kalio la Jino

Kalamu yamwaga wino, domo achamo la meno,
Peputoko la kiuno, ng’ang’ano kubwa la kono,
Maisha hisia duni, mithili jiko la kuni.

Maisha hisia duni, mithili jiko la kuni,
Karatasi na uneni, mengi toka kalamuni,
Maneno kuwa ajali, kichwani kutunza kweli.

Maneno kuwa ajali, kichwani kutunza kweli,
Kinywani fumbo jabali, kwa weledi jikubali,
Wino wasema ya mwili, pepo zote kukabili.

Wino wasema ya mwili, pepo zote kukubali,
Kati ya moja na mbili, namba gani huna huli?
Wewe mwana wa johari, mpenda zote fahari.

Wewe mwana wa johari, mpenda zote fahari,
Utunzapo zako siri, maishayo waathiri,
Maisha kweli bahari, kugida kwingi kuzuri.

Maisha kweli bahari, kugida kwingi kuzuri,
Kisimani kwa uturi, jazo zenye njema buri,
Kalamu sasa andiko, toto lake la kijiko.

Kalamu sasa andiko, toto lake la kijiko,
Yatima mwendo wa koko,mitaani na tandiko,
Gemagema nung’uniko, fahari zote si zako.

Gemagema nung’uniko, fahari zote si zako,
Pekee kalamu yako, wajane wa nyendo zako,
Agizo kuwa tambuzi, kama vilio vya mbuzi.

Agizo kuwa tambuzi, kama vilio vya mbuzi,
Ama checheto za kuzi, mithili kuno la mbuzi,
Kazi ng’amuo la tezi, ulimwengu ulowezi.

Kazi ng’amuo la tezi, ulimwengu ulowezi,
Damu chemko la kazi, maisha kuwa chukuzi,
Athari kuwa chirizi, nukio zake mafyuzi.

Athari kuwa chirizi, nukio zake mafyuzi,
Kamatio la kalizi, maisha ungo la uzi
Jino kalio la fizi, akili ya dudumizi.

Tamati mwisho mwa wino, kalio la fizi jino,
Domo achamo la meno, fizi kalio la jino,
Maisha nyanyaso kono, masikini ungo uno.

Abed Anthony
(Shimbolyo)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!