Nisikilize Mwanangu

Mwanangu nakuhusia, sikia yangu kalima,
Sipendi uje umia, moyo ukaja niuma,
Neno langu shikilia, mbele likufae vyema,
Waja hawanao wema, jichunge usije zama.

Hii ya kwetu dunia, inayo nyingi lawama,
Wengi waweza kujia, ukajawa na huruma,
Kumbe wanalonuia, ni kukutoa uzima,
Waja hawanao wema, jichunge usije zama.

Kwanza embu fikiria, fanya vyema kuwasoma,
Penye dosari kimbia, bila kugeuka nyuma,
Wala usije jutia, ati wataja kusema,
Waja hawanao wema, jichunge usije zama.

Japo watakutungia, wao mwingi uhasama,
Na watakufanyizia, za kwao nyingi hujuma,
Ila wewe vumilia, ivuke yote milima,
Waja hawanao wema, jichunge usije zama.

Waweza kukunuia, kwa mtego wa ndarama,
Ili ukishaingia, itimiye yao njama,
Amini nakuambia, hautatoka salama,
Waja hawanao wema, jichunge usije zama.

Usipo yashikilia, ukaishi kama kima,
Utakupata udhia, na dawamu utakwama,
Bora ufyate mkia, hivi kungali mapema,
Waja hawanao wema, jichunge usije zama.

Kaditama naishia, kwenye kituo nakoma,
Salamu nakutumia, kwa hii yangu nudhuma,
Heri kujihifadhia, hadi siku ya kiyama,
Waja hawanao wema, jichunge usije zama.

© Kinyafu Marcos,2018.
(Muumini wa kweli),
Dar es salaam, Tanzania.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!