Tunda la Mti Kati

Lilimponza Adamu, dhambini kuangukia,
Wakwanza binaadamu, Mungu alomchagua,
Kalila kwa zake hamu, sa wote tunahatia,
Ni tunda la mti kati.

Walisumbua fahamu, maswali kujijazia,
Kwani kuliweka humu, kama tunda la kuua?
Hamfi na mtadumu, nyoka aliwaambia,
Ni tunda la mti kati.

Lilionekana tamu, wakashindwa vumilia,
Wakasahau nidhamu, Mungu kumpotezea,
Hawakuona ugumu, bali utamu kolea,
Ni tunda la mti kati.

Mola aliwaazimu, mti kati ku’kataa,
Hawa kwa mashamushamu, wa kwanza kupuuzia,
Kala kaona utamu, mumewe akamgea,
Ni tunda la mti kati.

Tunda siyo la msimu, machoni linavutia,
Halitaki marhamu, ili lipate nukia,
Wakala wendawazimu, janga likawashukia,
Ni tunda la mti kati.

Nyoka wakamlaumu, kwani aliwapotoa,
Porini pakawa sumu, Mungu aliwaondoa,
Na tena umerehemu, kwao uliwajilia,
Ni tunda la mti kati.

Naleta yangu nudhumu, moyoni nikiumia,
Hali zimekuwa ngumu, kukoma kujishaua,
Tungekua masanamu, tunda tusingetumia,
Sasa kwalo twajikimu, yani lishatuzuzua.

© Alvin Aron
Tunevin

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!