Mke wa Mtu ni Sumu

Ni sumu kama ya bafe, simkonyezee katu,
Na wala chake kitufe, sikibonyeze mwanetu,
Sije we bure ukafe, kisa ni mke wa mtu,
Mke wa mtu ni sumu, jiepushe naye kaka.

Usichekecheke naye, nakukanya mwafulani,
Songa mbali sana naye, kamwe usimtamani,
Na simu simpigiye, mchana wala jioni,
Mke wa mtu ni sumu, jiepushe naye kaka.

Hata ajapo kujia, akiwa melowa chozi,
Sidhubutu nakwambia, kumwimbia bembelezi,
Mtegoni sijengia, kwa kujifanya mwokozi,
Mke wa mtu ni sumu, jiepushe naye kaka.

Asije kukuhadaa, kwa manenoye matamu,
Eti mume hatajua, akakupa vya haramu,
Gizani ukapapia, huku ukilishwa sumu,
Mke wa mtu ni sumu, jiepushe naye kaka.

Kaburi sijichimbie, mke wa mtu kupenda,
Mwisho wake ujifie, kama nzi kwa kidonda,
Nishakukataza mie, mke wa mtu kuganda,
Mke wa mtu ni sumu, jiepushe naye kaka.

Jitafutie wa kwako, wa wenyewe siendee,
Mlete nyumbani mwako, mahari umlipie,
Wamjue ndugu zako, chakula awapigie,
Mke wa mtu ni sumu, jiepushe naye kaka.

© Bonface Wafula
(Mwana Wa Tina) Lanet, Nakuru, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!