Juhudi ni Nguzo

Nimefika kwenu hapa, nimeleta yangu hoja,
Mawaidha nitawapa, nizikidhi zenu haja,
Katu siwatoi kapa, Hoja yangu ina tija,
Juhudi jamani nguzo, uvivu tuupingeni.

Juhudi daima kinga, yakufikia malengo,
‘Kitenda bila kulinga, utatimiza mipango,
Juhudi hii nalonga, inanusuru vifungo,
Juhudi jamani nguzo, uvivu tuupingeni.

Juhudi katika kazi, yatakiwa hasa hasa,
Achana nayo ajizi, ili usije jitosa,
Usifanye kama ya juzi, wakati wako ni sasa,
Juhudi jamani nguzo, uvivu tuupingeni.

Fanya kazi bila hofu, gangamala hadi mwisho,
Hata iwe njia ndefu, usitishwe na vitisho,
Tenda yote kwa unyo’fu, usingoje ije kesho,
Juhudi jamani nguzo, uvivu tuupingeni

Juhudi tuiongeze, sote kwenye kazi zetu,
Katu tusiipunguze, hii ndiyo nguzo yetu,
Uvivu tuukimbize, kamwe usikae kwetu,
Juhudi jamani nguzo, uvivu tuupingeni.

© Kinyafu Marcos

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!