Balaa Itawapata

Nilizipata habari, tokea kule shuleni ,
Shule zimo kwa hatari, zawashwa moto gizani ,
Nini hasa mwafikiri, muwashe moto shuleni ,
Balaa mwaitafuta, na kweli itawapata.

Sikieni wanafunzi,mlipelekwa shuleni ,
Mkapewa moja kazi, msome vitabu tani ,
Nayo ni rahisi kazi, isiwashinde jamani ,
Shule mnapozichoma, balaa itawapata ,

Shule mkizichoma, mwatuvuruga vichwani,
kwani mwafaa kusoma, mkiwa huko shuleni ,
Lakini sio kuchoma, msomeako jamani ,
Balaa mwaitafuta, na kweli itawapata.

Msiwe na wasiwasi, mtapita mitihani ,
Msiwe kama waasi, maovu kuyatamani ,
Mitihani ni rahisi, wanafunzi kumbukeni ,
Shule mnapozichoma, balaa itawapata .

Sisi wazazi twalia, machozi yamo machoni ,
Tabu mmetuletea, mkiwa bado shuleni ,
Nanyinyi mtalipia, kwa kuyachoma mabweni ,
Balaa mlitafuta, na kweli itawapata .

Simama wima simama, utweleze hadharani ,
Bada ya skuli kuchoma, umepata raha gani ,
Umepata yepi mema, ya furaha maishani ,
Shule mnapozichoma, balaa itawapata.

Mengine sitaongeza, kalamu naweka chini ,
Nikiwaomba kuwaza, hasa walio shuleni ,
Shule kuteketeza, faida yake ni gani? ,
Balaa mlitafuta, na kweli itawapata.

© Stephen Muia Musau
(Malenga Mneni) Juja, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!