Tega Sikio

Sikia e ndugu yangu,nikwambie kwa uzuri,
Sikia mja mwenzangu, sikia na kufikiri,
Ni kwanini walimwengu, tumejawa na viburi,
Yanini kusengenyana, sote tukifa twanuka.

Dunia ‘meharibika, umoja haupo tena,
Upendo umetoweka, twaishi tukisemana,
Wapi tunajipeleka, nambieni waugwana,
Yanini kusengenyana, sote tukifa twanuka.

Tulio jaliwa mali, twadharau masikini,
Kiburi kwetu asili, wala haya hatuoni,
Kauli zetu ni kali, zaumiza mitimani,
Yanini kusengenyana, sote tukifa twanuka.

Walojaliwa visomo, vya ilimu darasani,
Kundi hili nao wamo, wadharau hadharani,
Kwa kejeli na misemo, ni mabingwa mtaani,
Yanini kusengenyana, sote tukifa twanuka.

Manani alituumba, sote sisi mali yake,
Naye amesema kwamba, pendo lake tulishike,
Wala tusije jigamba, tukapigana mateke
Yanini kusengenyana, sote tukifa twanuka.

Kuna siku tutakufa, hilo wote tukumbuke,
Zisitutawale sifa, tukajitia makeke,
Yatatufika maafa, na peponi tusifike,
Yanini kusengenyana, sote tukifa twanuka.

Nawakumbusha tutubu, sote tumeshakosea,
Sote kwakila dhehebu, tusi’shi kwa mazoea,
Isitufike adhabu, wote tukaangamia,
Yanini kusengenyana, sote tukifa twanuka.

Kweli tuishi kwa toba, kwa mapenzi yake Mungu
Hii itakuwa tiba, tuyaepuke majungu,
Ili tufike kwa Aba, muumba wa ulimwengu.
Yanini kusengenyana, sote tukifa twanuka.

© Kinyafu Marcos

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!