Vipawa Tuvitumie

Enyi vijana wenzangu, sikizeni kwa makini,
Ulio ujumbe wangu, ujumbe toka moyoni,
Kipawa cha mlimwengu, tukitile maanani,
Vipawa tukitumia, tutapata kufaidi.

Kila siku ni machozi, machozi kwetu machoni,
Twaomba usaidizi, mpaka serikalini,
Kulia hamna kazi, basi vipawa vya nini?
Vipawa tukitumia, tutapata kufaidi.

Katujalia Jalali, vipawa kwetu nafsini,
Navyo huwa mbalimbali, vijana tukumbukeni,
Ili tuboreshe hali, hali zetu za nyumbani,
Vipawa tukitumia, tutapata kufaidi.

Tukitumia vipawa, vijana nisikizeni,
Umaskini takuwa, haumo tena nchini,
Nazo kazi zitakuwa, darahimu mifukoni,
Vipawa tukitumia, tutapata kufaidi.

Najua mwanielewa, nisemacho ndicho nini,
Kwa kuwa ni sisi haswa, tutesekao nchini,
Kwa kukosa kazi sawa, tuzitakazo moyoni,
Vipawa tukitumia, tutapata kufaidi.

Kipawa ndicho kipawa, hakuna kilo cha chini,
Vinatoshana vipawa, hakuna kilicho duni,
Ulichonacho kipawa , kitilie maanani,
Vipawa tukitumia , tutapata kufaidi .

Wengi watakudunisha, usikate tumaini,
Neno la kukudunisha, usiliweke moyoni,
Lisije likakufisha, na u hai duniani,
Vipawa tukitumia, tutapata kufaidi.

Vijana ukacha woga, utakuwa rizikini,
Kipawa chako ‘kijenga, utapata burudani,
Hivyo jenga pasi woga, bila kujali waneni,
Vipawa tukitumia , tutapata kufaidi.

Wanao kushauri, watilie maanani,
Wataka uwe wa kheri, bila kilio machoni,
Hivyo shika ushauri, usipotee njiani,
Vipawa tukitumia, tutapata kufaidi.

Kalamu nabwaga chini, ndimi malenga mneni,
Vijana nawaauni, vipawa si vya utani,
Tuvitumie nchini, twache kuwa duniduni,
Vipawa tukitumia, tutapata kufaidi.

© Stephen Muia Musau

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!