Kamari Kamaliza

Kuna jambo nalikiri, maradhi yamesambaa,
Ya wazi tena si siri, kote yanazua waa,
Gonjwa hili nafikiri, metugeuza vichaa,
Hili jambo la kamari, linakula halisazi.

Wamejawa na ghururi, daima watuhadaa,
Tena wapaka uturi, kamari ipate ng’aa,
Kumbe ina takisiri, wanatuzulia baa,
Hili jambo la kamari, linakula halisazi.

Si uongo ni dhahiri, nyumba nyingi zina njaa,
Darahima nafikiri, kamari zimezitwaa,
Zilizobaki shubiri, moyoni zimetujaa,
Hili jambo la kamari, linakula halisazi.

Serikali tusitiri, iturejee shifaa,
Maisha yawe ya kheri, ituondoke balaa,
Makampuni maayari, waache kutuhadaa,
Hili jambo la kamari, linakula halisazi.

Nawapeni ushauri, jukuani nikipaa,
Tuwaacheni kamari, tusigeuke vichaa,
Kamari si takidiri, Mungu analikataa,
Hili jambo la kamari, linakula halisazi.

© Moses Chesire

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!