Luthuli Tumepajua

Pale dukani luthuli, mshamba niliingiani,
Nilimkuta tapeli, mwenye maninga makini,
Luthuli tumepajua, wahuni mumebanana.

Alikaribisha pale, dukani alikokuwa,
Hakuwa nayo kelele, mpole falau njiwa,
Akaniza upole, nilichotaka kuuziwa,
Luthuli tumepajua, wahuni mumebanana.

Kijinga nilifurahi, nikadhani naenziwa,
Wateja anawastahi, nikasema kwa fahiwa,
Sikujua nikebehi, mwenzenu naadaiwa,
Luthuli tumepajua, wahuni mumebanana.

Nataka televisheni, kubwa na yakuvutia,
Nikamwambia mhuni, mshamba nikichekea,
‘takugharimu mapeni, msela akanambia,
Luthuli tumepajua, wahuni mumebanana.

Riale nikazitoa, nikaweka mkononi,
Nikapawa ya bandia, sio  niliulizani,
Kwa uchungu nikalia, naibiwa masikini,
Luthuli tumepajua, wahuni mumebanana.

Polisi nikafikiri, watanifaa kikweli,
Nikafyatuka kingiri, moyoni nikisaili,
Hatimaye nikakiri, zimepotelea mbali,
Luthuli tumepajua, wahuni mumebanana.

Wakenya nisikizeni, Luthuli kunao wezi,
Sio moja ni miteni, wanaiba waziwazi,
Mitambo ukitakani, wahindi hutoki chozi,
Luthuli tumepajua, wahuni mumebanana.

© Moses Chesire (Sumu ya waridi) Kitale