Ewe Kinda

Jaza uso tabasamu,na furaha waziwazi,
Ni mie wako adimu,nikwitae laazizi,
Umenitia wazimu,wakosesha usingizi,
Nakuwaza kwa hamumu,uwe wangu muuguzi,
Nikupacho ni kionjo,malavidavi ndo bado.

Kidosho umerembeka,nakuwaza kila saa,
Na mapenzi kuropoka,menifanya kuduwaa,
Nakwambiya malaika,wewe kwangu si balaa,
Ndiposa nalumbika,na kukupa la wasaa,
Nikupacho ni kionjo,malavidavi ndo bado.

Nijuacho mia mia,kwa mapenzi meanguka,
Kukupata maidia,moyo wangu melipuka,
Kukuwaza nakimbia,sijui nikuchizika?
Kuwa wangu malkia,kuwa nawe sitochoka,
Nikupacho ni kionjo,malavidavi ndo bado.

Meniacha ninalia,penzi lako si mfano,
Sikumoja tatujia,itakuwa mauano,
Sitosita kumbatia,hata iwe minong’ono,
Kidege wangu sikia,kwako bado mapambano,
Nikupacho ni kionjo,malavidavi ndo bado.

Niamini nakupenda,penzi lako sitorusha,
Wacha live kama tunda,maji yake takunywesha,
Penzi letu kiliponda,itakuwa kujichosha,
Laishia na kuvunda,kwa raha kuitorosha,
Nikupacho ni kionjo,malavidavi ndo bado.

Kiditamati mpenzi, kalamu natia nanga,
Ni bahati kuwa manzi,kwani mola alipanga,
Takulipa kwa ulinzi,maadui wakipinga,
Kipendacho roho mwenzi,hula nyama mbichi panga,
Nikupacho ni kionjo,malavidavi ndo bado.

© Brian Mutambo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!