Vita

Kitu baya duniani,ni vita vinapojiri,
Hukosesha na amani,swala hili ni hatari,
Hutuacha na huzuni,hata wale matajiri,
Amani haiji jamani,kwa ncha ya upanga.

Kwa ncha ya upanga,huzidi tena vibaya,
Hudhaniwa ni kupanga,watu wengi hujifiya,
Na kuzidisha matanga,halaiki jihamiya,
Kina mama tangatanga,na watoto vile vile.

Na watoto vilevile,elimu kuwakosesha,
Yatima wawachwa pale,hadhi yao kukosesha,
Na upweke zidi wale,wabakio vita isha,
Ni furaha ya kunguru,vita vya panzi kwa kweli.

Vita vya panzi kwa kweli,maadui hufurahi,
Hunyakua shamba mali,kila kitu wakawahi,
Vita vikiwa mahali,hukosesha na sabahi,
Hakuna ano kujali,hataawe ni jirani.

Hata awe ni jirani,aweza kukusaliti,
Aje kwako masikani,kuvamia na umati,
Hata uwe msalani,vita kija ni mauti,
Vita macho havinani huanzia kwa ugomvi.

Huanzia kwa ugomvi,na baadaye ni kisasi,
Mambo hugeuzwa chumvi,mapigano kwa risasi,
Mie nafungua jamvi,na kuanza ukasisi,
Sinione sina mvi,nakanya ya vita koma.

Nakanya ya vita koma,hasaa ya kikabila,
Hivi huleta na homa,hutuacha  mali bila,
Nao waja kulalama,kupoteza yao mila,
Buheri mie nasema,amani ni dawa bora.

Amani ni dawa bora,huleta utangamano,
Demokrasia ni kwa kura,wanasiasa mashindano,
Tubadili hino sura,ya kuwepo mapigano,
Tamatini ninahora,nawaacha kwa maono.

© Brian Mutambo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!