Taifa ni Maadili 

Naingia ukumbini, nyote kuwakariria,
Ushairi niwapeni, hoja nitawaachia,
Mnipe masikioni, ‘shike nachoelezea,
Taifa sio taifa, pasi kuwa maadili.

Naanza kwa uzalendo, nchi yetu tuipende,
Yadhihirishe matendo, nchi yetu tuilinde,
Wa kila mtu mwenendo, usije kawa mpinde,
Taifa sio taifa, pasi kuwa maadili.

Wote tuwe na umoja, tuuache ukabila,
Kabila lisiwe hoja, mwenza kumnyima hela,
Taifa letu ni moja, Mkenya ndilo kabila,
Taifa sio taifa, pasi kuwa maadili.

Linda demokrasia, uongozi tushiriki,
Haki kujielezea, wachotaka na hutaki,
Changu naweza tetea,  demokrasia haki,
Taifa sio taifa, pasi kuwa maadili.

Tena adili usawa, mgao raslimali,
Bajeti inapogawa, isawazishe ratili,
Idara zilizoundwa,’faidi kila mahali,
Taifa sio taifa, pasi kuwa maadili.

Tuwe na uadilifu, twache tamaa ya hongo,
Tusiwe na udhaifu, wa kuwa watu waongo,
Tukomeshe uhalifu, kisha tuache maringo,
Taifa sio taifa, pasi kuwa maadili.

Na inavyoelezea, katiba ni kielezi,
Tutii kwa mazoea, hadi kijacho kizazi,
Kwa hayo nitamwachia, hiyo ya ziada kazi,
Taifa sio taifa, pasi kuwa maadili.

© SAMWEL MWANGI GATHIA

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!