Wajanja Hatari

Imezuka sarakasi, tumeona paruwanja,
Wanakulana mafisi, walojidhani wajanja,
Kwa vijembe na matusi,wenyewe wanajichanja,
Hicho kilimo mahindi, kitawatoka puani.
Blogu ya Mashairi
Imezuka sarakasi, tumeona paruwanja,
Wanakulana mafisi, walojidhani wajanja,
Kwa vijembe na matusi,wenyewe wanajichanja,
Hicho kilimo mahindi, kitawatoka puani.
Wawapi mahayawani, wale tulowaamini,
Ola wanavyotuhini, sisi tulomasikini,
Tuliwatia moyoni,tukidhani ikhiwani,
Nimekiri ya wahenga, kikulacho ki nguoni.
Uliye wangu Wadudi, muumba wa roho yangu,
Kwako leo ninarudi, usikie taabu zangu,
Kama ni kombo ni rudi, kwani ndiwe Mungu wangu,
Nilinde wangu Wadudi, dhidi ya nafsi yangu.
Ijapo si mtambaji, nitakuli kwa katiti,
Wala sitafuti taji, musinipige vijiti,
Ningependa kuwahoji, hawa wavaa taiti,
Zingwizingwi lipe nguo, uyaone mashauo.
Nashukuru usokoma, hapa nilipopafika,
Moyoni nina naima, tena isomithilika,
Ulonitenda ni mema, ewe uliye rabuka,
Nakurejea Rabuka, mimi wako mpotevu.
Jana ndoto linijia, kote kumejaa damu,
Sijui likotokea, tena yao binadamu,
Mana nalisubiria, meuliza wanajimu,
Waganga naulizia, kitale lama lamu.
Nawataka na magunge, wajenifunza kutunga,
Napo tunga nizitunge, zilotungwa kama shanga,
Mishororo niipange, pasi wazo kubananga,
Na waje walo magunge, njia kunimulikia.
Nawaita ikhiwani, kitaka muwe majaji,
Sikiza nielezeni, utamu wangu mlaji,
Lipo hapa kiganjani, li tamu kama kileji,
Napenda tikitimaji, tunda bora shinda zote.
Unaweza kupata App yetu mpya kutoka kwa Google Play Store na uweze kulisoma shairi hili vizuri kwa simu yako au kulihifadhi usome baadaye bila mtandao