Jahazi la Mwanaume 

Ewe sikiliza haya, yaloleta mjadala,
Bada tendo lenye haya, liporipoti makala,
Mwanamume jiteteya, na ufanye halahala,
Jahazi la mwanamume, nani ataliokoa?

Nyumbani ovyo kupigwa, na bibiyo ni aibu,
Nyumba kwako kukaliwa, hiyo si ni masaibu,
Kwani wewe kaolewa, jinako waharibu,
Jahazi la mwanamume, nani ataliokoa?

Meingiliwa mabwana, ila wengi mnakana,
Kazini mwakazana, ila na mali huna,
Nyumbani bibi anena, na wewe maneno huna,
Jahazi la mwanamume, nani ataliokoa?

Mwanamume ni kushika, ushukani hiyo doa,
Usitafute talaka, mke kitaka odoa,
Nyumbaniko wajibika, hilo litaishi doa,
Jahazi la mwanamume, nani ataliokoa?

Mwanamume na si jasho, kama wengi wasemavyo,
Ila bado si vitisho, kila pahali ‘takavyo,
Kitalakiwa si mwisho, ijapo pokea hivyo,
Jahazi la mwanamume, nani ataliokoa?

Mwanaume si usherati, kila mbinti wataka,
Jihadhari maiti, ama utafa haraka,
Hayo tapata tikiti, kuenda ahera kitaka,
Jahazi la mwanamume, nani ataliokoa?

Mwanamume si kukunywa, pombe bila kipimo,
Kila wakati kulewa, hata unalala shimo,
Klabuni msemo “pewa”, kiwika chako kidomo,
Jahazi la mwanamume, nani ataliokoa?

Wanaume samahani, ju ya kuwaingilia,
Ila niliona soni, kaona sitaachia,
Hizo hisia moyoni, ila naziachilia,
Jahazi la mwanamume, nani ataliokoa?

© SAMWEL MWANGI GATHIA

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!