Kilio cha Haki

Hii leo nahakiki, mnyonge hanayo haki,
Angangana kisamaki, alowekwa maji jiki,
Asumbuka tika dhiki, kwa kunyimwa zake haki,
Ninalia kwa hamaki, kulilia zetu haki.

Ninayo tele machungu, kwao wale askari,
Bila kosa kanipingu, kwa kutowapa asari,
Kutopatiana changu, nikawekwa kwa hatari,
Ninalia kwa hamaki, kulilia zetu haki.

Kwingine ni kwa ofisi, matendo mekuwa hasi,
Kama wewe huna kasi, ya mwenendo wa kuasi,
Kitu kidogo si ‘tesi, leo ni hali halisi,
Ninalia kwa hamaki, kulilia zetu haki.

Mgonjwa sipitalini, tibabu sawa hapati,
Zahepa kichinichini, ni dawa hata za miti,
Wasimamizi wahuni, mbona sinyang’anywe vyeti?
Ninalia kwa hamaki, kulilia zetu haki.

Mnyonge kuwa na haki, hicho mekuwa kizungu,
Kwa zile hajui haki, anapitia machungu,
Naomba apewe haki, hilo ombi kwake Mungu,
Ninalia kwa hamaki, kulilia zetu haki.

© Samwel Mwangi Gathia

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!