Sauti ya Ukombozi

Kuniradhi mwenzangu, sikia haya maneno,
Jalali Mwenyezi Mungu, akupenda tena mno,
Ingawa una machungu, fikiri mema maono,
Sauti ya ukombozi, isikie wazi wazi.

Taabu umepitia, mara mingi wateseka,
Tumaini lazimia, kwa liyopita miaka,
Hata ukawachilia, maishako yakatika,
Sauti ya ukombozi, isikie wazi wazi.

Baada kupata dhiki, faraja hukuadama,
Ni  ukweli mantiki, mwenye busara kasema,
Shida nyingi kila wiki, siku moja yatakoma,
Sauti ya ukombozi, isikie wazi wazi.

Mpanda ngazi hushuka, leo hoi kesho heri,
Ayubu aliteseka, hata ikawa desturi,
Maradhi yakamshika, na hakukana Jabari,
Sauti ya ukombozi, isikie waziwazi.

Waliofaulu leo, walianza kwa taabu,
Hayakuwa mazuio, kufaulu kwa ajabu,
Walipata azimio,kutoka kwa madhehebu,
Sauti ya ukombozi, isikie wazi wazi.

Asante kwa kusikia, hayo nimekueleza,
Natamani utaweza, baada ya kuyawaza,
Kuamua kupuuza, ama nilivyoeleza,
Sauti ya ukombozi, isikie wazi wazi.

© SAMWEL MWANGI GATHIA

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!