Magaidi Janga

Nimejawa na ghadhabu, sababu ya magaidi,
Wakatili al-shababu, matendo yao mezidi,
Kuua bila aibu, si ishara ya ushindi,
Nendeni kwenye vita, mkapigane na jeshi.

Likuwa Mpeketoni, leo hii mko Garisa,
Tukisali kanisani, mnakuja kututesa,
Tunaishi uogani, ila hatuna makosa,
Kuwaua waso kosa, nalaani hilo tendo.

Na hii so mara ya Kwanza, ila mezidi unga,
Na tangu walipoanza, twashinda kwenye matanga,
Rabana twapoteza, Wakenya kwa hili janga,
Turehemu Rabana, tulinde ewe mwenyezi.

Ninawapa changamoto, Wakenya na serikali,
Kukabili hili joto, kwa hatua kali Kali,
Dawa ya moto ni moto, pia watendwe katili,
Kiweka chini kiboko, mtoto amea pembe.

Kwake raisi waraka, sababu ndiye kamanda,
Atumie madaraka, wanajeshi wengi kwenda,
Kulinda yetu mipaka, ili zipungue shida,
Kamwe wasiweze penya, kukuja hapa nchini.

Miye kwa niamba yangu, ninatoa rambirambi,
Natoa kwa uchungu, ujumbe huu kwenye ukumbi,
Kisali kwa yeye Mungu, uwaenee kama vumbi,
Jamaa wa waathiriwa, pole zangu ziwaendee.

© SAMWEL MWANGI GATHIA

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!