Jihadhari za Bwerere 

Leo ni nyingine siku, naadika kueleza,
Nilofikiri usiku, watu wanavyoteleza,
Vyovyote vya bure huku, Wakenya mate kumeza,
Za bwerere jihadhari, za bwerere ni hatari.

Kukitendeka ajari, nafasi yenu kuvuna,
Lile la mafuta gari, kianguka pato pana,
Pasipo kujitahadhari, mwenda kuyachota tena,
Za bwerere jihadhari, za bwerere ni hatari.

Mwajitia mapuuza, somo hamjalipata,
Maisha mnayacheza, mnavyopiga ukuta,
Moto tawateketeza, viwete mkajipata,
Za bwerere jihadhari, za bwerere ni hatari.

Yawapo maadamano, huwa nyingine nafasi,
Kupora vitu vitano, kwa ulafi wa kifisi,
Ni buheri mikutano, kutengeneza nafasi,
Za bwerere jihadhari, za bwerere ni hatari.

Usiku sina amani, siupati usingizi,
Sio ilivyo zamani, kulingana na ya juzi,
Utajiri sitamani, sasa kuna wingi wizi,
Za bwerere jihathari, za bwerere ni hatari.

Na hata hayo masomo, bure mwataka kupasi,
Bila kuwa mtazamo, La ‘mwakenya’ haufasi,
Nautangaza mgomo, wizi huo kuuasi,
Za bwerere jihadhari, za bwerere ni hatari.

Nyuma katu kuachwa, wanasiasa kwa kasi,
Mna bidii za mchwa, kupata pato kiasi,
Mali ya umma yafichwa, hayatufaidi sisi,
Za bwerere jitahadhari, za bwerere ni hatari.

Nawasihi mubadili, muwe wastaarabu,
Tusiongozwe na mali, faidika kujaribu,
Tuishivyo kwa ukali, ungwana uwe karibu,
Za bwerere ni hatari, za bwerere ni hatari.

© Samwel Mwangi Gathia

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!