Utungapo Mashairi

Ukitunga mashairi, waulize wakufuu,
Wakufuu ‘ki’hakiri, utatunga tungo vuu!
Tungo vuu! sio zuri, nyingi zazo ni upuu,
Waulize wakufuu.

Ukitunga mashairi, uepuke uchokoo,
Uchokoo ni hatari, huibua fondogoo,
Fondogoo ‘kishamiri, itanuka kama choo,
Uepuke uchokoo.

Ukitunga mashairi, na sheria uzitii,
Uzitii nakariri, na utunge kwa bidii,
Kwa bidii na uturi, yapendeze wengi ndii,
Na sheria uzitii.

Ukitunga mashairi, utunge ya kipekee,
Upekee udhihiri, yapendeze waja tee,
Waja tee washakiri, kwa mafunzo yako shee,
Utunge ya kipekee.

Ukitunga mashairi, hakikisha yatafaa,
Itafaa uhariri, tungo zako kila saa,
Kila saa mashauri, usikose kuyatwaa.
Hakikisha yatafaa.

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!