Naulizia Mizimu 

Nalisogeza suali, kwenu watu mashuhuri,
Munipe jibu la kweli, wala musinihakiri,
Mulo karibu na mbali, munipe jibu la heri,
Naulizia mizimu,i wapi nikaizuru?

Nende kwayo siku mbili, nikatulize akili,
Nepuke huu muhali, ulojitoa sabili,
Nendapo kila mahali, naona vimulimuli,
Naulizia mizimu,i wapi nikaizuru?

Nimekwenda sipitali, sijapata dawa shwari,
Mbinu zote zimefeli, nyingi zimeleta shari,
Nalala kichalichali, tumbo limefura furi,
Naulizia mizimu,i wapi nikaizuru?

Nahisi kisulisuli, medhofika wangu mwili,
Ndwele imeyakabili, maungo ‘ngu mbalimbali,
Siku hizi hata sili, bovu sana yangu hali,
Naulizia mizimu,i wapi nikaizuru?

Ni bovu sana amali, ya wetu madakitari,
Kwanda wanoe makali, watwepushie hatari,
Mizimu ni afadhali, itan’ondolea shari,
Naulizia mizimu, i wapi nikaizuru?

Ninavyo visu viwili, ndani ya wangu muili,
Tabibu mwenda sukuli, aliviacha na kuli,
Mepita myaka miwili, bado nasitahimili,
Naulizia mizimu,i wapi nikaizuru?

Kaditama nasaili, munipe yenu habari,
Hata ikiwa i mbali, nitaizuru nakiri,
Mekonda sina mithili, siha yangu sio zuri,
Naulizia mizimu,i wapi nikaizuru?

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!