Ua Langu Nudhumu

Ua nasitajabia, vile unavyonukia,
Ua napokwangalia, nahisi kujizimia,
Ua nikikusogea, moyo wangu hutulia,
Ua langu nuudhumu, huishi kunivutia!

Ua jua liki’ngia, taratibu wachanua,
Ua jua likitua, kikonyo wakifungia,
Ua kwenye langu pua, harufuyo nasikia,
Ua langu nuudhumu,huishi kunivutia!

Ua wanisisimua, maungo na damu pia,
Ua na zangu hisia, unapenda kuchezea,
Ua lau ungejua,namna livyokugandia,
Ua langu nuudhumu,huishi kunivutia!

Ua giza likingia, na lala kikuwazia,
Ua nakutamania, kwako miye nimetua,
Ua kwako medatia, na siwezi jinasua,
Ua langu nuudhumu, huishi kunivutia!

Ua kinikatalia, miye nitajifilia,
Ua kininyamazia, moyoni nitaumia,
Ua ninasubiria, siku tutafunga ndoa,
Ua langu nuudhumu, huishi kunivutia!

Ua tungo nakomea, najua utawazia,
Ua mi peke najua, jinsi navyokupendea,
Ua ninakungojea, au machozi ta’ngua,
Ua langu nuudhumu,huishi kunivutia!

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!