Afadhali

Afadhali saratani, iuwayo wanadamu,
Wakatiwa kaburini, na kukosa umuhimu,
Kuliko hichi kiburi, kiloshika binadamu!

Afadhali masikini, aishiye kibandani,
Akosaye aswilani, vya msingi maishani,
Kuliko huyo tajiri,kulla siku anahini!

Afadhali huyo mwana, arandaye mitaani,
Leoni na pia jana, ajiliya vya jaani,
Kuliko huyo jeuri,afisidi taifani!

Afadhali makafiri, wasoenda mabadini,
Kulla siku washamiri, vilabuni majijini,
Kuliko anohubiri,na usiku yuwazini!

Afadhali visabalu, waishio vilabuni,
Wava’o pambo za lulu, kunasa walo njiani,
Kuliko wanohakiri, na kuchepuka ndoani!

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!