Vya Thamani Matopeni

Kitu kilo cha thamani, cha thamani sikizeni,
Takipata kilindini, kilindini huko chini,
Hutopata lulu cho’ni, lulu cho’ni huioni!
Vya thamani matopeni, matopeni huvipati.

Wengi wa’ga duniani, duniani waukeni,
Bila lulu kuoneni, kuoneni aswilani,
Vya thamani ‘limwenguni, ‘limwenguni vifichoni,
Vya thamani matopeni, matopeni huvipati.

Alimasi dhahabuni, dhahabuni naambeni,
Huvipati mchangani, mchangani na njiani,
Au huko mitaani, mitaani mitaroni,
Vya thamani matopeni, matopeni huvipati!

Kaviumba Maanani, Maanani kaumbeni,
Utosini unyayoni, unyayoni kawekeni,
Wanadamu siku hini, siku hini wa’nikeni,
Vya thamani matopeni, matopeni huvipati!

Vya thamani na machoni, na machoni huvioni,
Vya funikwa wenzanguni, wenzanguni vi fichoni,
Na visivo na thamani, na thamani vi wazini,
Vya thamani matopeni, matopeni huvipati!

Vipo vingi maishani, maishani vilo duni,
Kona zote taifani, taifani vi pomoni,
Tavipata madukani, madukani shubakani,
Vya thamani matopeni, matopeni huvipati.

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!