Tuwafae Maskini

Sidharau mwenye njaa, eti hana manufaa,
Huyo aso na shufaa, taifani ndiye taa,
Ni vizuri kumfaa, umwondowe kwenye baa,
Huyo muuza makaa, ipo siku atapaa!

Ukimwona kwenye jaa, taka akichokoraa,
Jua ni yako adaa, kumfaa mwenye njaa,
Huyo aliyechakaa, siku moya atang’aa,
Huyo muuza makaa, ipo siku atapaa!

Ndugu zangu ni wakaa, tuondowe hino baa,
Afrika imezagaa, imeshika ushukaa,
Wako wapi mashujaa? watufunze ujamaa,
Huyo muuza makaa,ipo siku atapaa!

Ni kwa nini mwaduwaa, ilhali ipo baa,
Sio vyema kuambaa, tuwafae wenye njaa,
Amukeni mlokaa, ili tukataataa,
Huyo muuza makaa, ipo siku atapaa!

So vyema kutunduwaa, tuondoweni mawaa,
Ukata ‘metapakaa, pembe zote umetwaa,
Huu ndo wetu wasaa, hamuna haja kuyaa,
Huyo muuza makaa,ipo siku atapaa!

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!