Wazee Tuwasikilize

Kuna wasoelezeka, wakaelewa bayana,
Hata ukawatandika, viboko na kuwakana,
Bado watakurupuka, kutenda yaso maana,
Waze’ tuwapulikize!

Huyu wa leo ‘sichana, ashiki mpenda raha,
Na waze’ akikosana, katu h’ombi msamaha,
Ajiona mwema sana, awajibu kwa madaha,
Waze’ tuwapulikize!

Maambo ya kifedheha, atenda bila makini,
Aonaa kama jaha, kuvalia bovu mini,
La mno kwake buraha, hajalishwi la usoni,
Waze’ tuwapulikize!

Huyu wa sasa ghulamu, hataki hata kusoma,
‘Kiambiwa la muhimu, adiriki ‘tusi mama,
‘Tashindwa kweli timamu, kila siku alalama,
Waze’ tuwapulikize!

Akataa palo pema, na andama mbaya ndiya,
Katu hataki gharama, apenda ya wepesiya,
Apenda kwa mama pima, anasa ndo aenziya,
Waze’ tuwapulikize!

Mwana mtukana nina, kuzimu enda kiona,
Wazazi ni wa thamana, tuwapulikize sana,
Jua ukiwatukana, taku’dhibu Maulana,
Waze’ tuwapulikize!

Kalamu naweka tini, himahima naondoka,
Tutiliye maanani, tuheshimu waswifika,
Wao kwanza ndo kiini, ndo maana tumefika,
Waze’ tuwapulikize!

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!