Wafileo Walifile

Yalopita sio ndwele, tugange yalo mbeleni,
Ndo kauli ya wavyele, tokea zao zamani,
Leo kipona upele, ujiandae tauni,
Wafileo walifile, mwoleza mfu ni nani?

Wandani na wasaile, tusahau ya zamani,
Mabaya yalo ya kale, tusiyatie moyoni,
Ni kama mavi ya kale,hayanuki aswilani,
Wafileo walifile,mwoleza mfu ni nani?

Yakija mapesa tele, yakufae maishani,
Yarudi yawe kichele, usiliye masikini,
Vyema uwe na sumile, utuliye akilini,
Wafileo walifile,mwoleza mfu ni nani?

Wapo kupe vitungule, wanjanja ulimwenguni,
Huongea polepole, wakunase mtegoni,
Lugha yao ni teule, yatoa nyoka pangoni,
Wafileo walifile, mwoleza mfu ni nani?

Na wakija kupe wale, wakunyonye muilini,
Usalie mchochole, usiliye masikini,
Masikini songa mbele, usahau ya zamani,
Wafileo walifile, mwoleza mfu ni nani?

Yakipita jipe kele, uandae ya usoni,
Maharagwe na mawele, uyapande mashambani,
Hayo ndiyo maumbile, kusahau ya zamani,
Wafileo walifile, mwoleza mfu ni nani?

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!