Njiwa Nakutuma

Njiwa enuka enenda, nenda kwa wangu lazizi,
Mwambe ninavyompenda, taratibu amaizi,
Mwambe moyo hunidunda, n’onapo yake mapozi,
Kovu lisimpe shaka, mueleze hilo wazi!

Njiwa enuka haraka, timka hadi Iteni,
Huko njiwa ukifika, yupo mrembo fulani,
Vizuri ameumbika, na ana ngozi laini,
Kovu lisimpe shaka, mueleze abaini!

Njiwa hebu usikize, huyo ni wangu muhibu,
Naomba ‘simchokoze, penzi letu kaharibu,
Mambo mengi usimuze, munenee kwa adabu,
Kovu lisimpe shaka,mueleze taratibu!

Njiwa shika hili ua, ndilo nililomwahidi,
Mwambie ukimpea, amenituliza fwadi,
Ni zuri linanukia, kuliko la halwaridi,
Kovu lisimpe shaka, muelezee,zaidi!

Njiwa muulize pia, aseme ni lini aja,
Maskini ninaumia, aje twishi pamoja,
Mwambie aje madia, niwe’kimpa pambaja,
Kovu lisimpe shaka,mueleze hiyo hoja!

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!