Hana Mtu Amuambe

Hana watu wampambe, maishani apambike,
Ameachwa autambe, mti ‘kavu peke pweke,
Tangu akiwa mkembe, ambiwa ‘sitetemeke,
Hana mtu amuambe, shidaze zitambulike?

Aambwa nd’o mwenyi pembe, amenyane kama jimbi,
Hapewi uki arambe, shubiri ndiye mrambi,
Bahari peke ayumbe, ang’eng’ane na mawimbi,
Hana mtu amuambe, nawauza ninyi wa’mbi?

Mwona heri myafumbe, macho yenu msimwambe,
Mwapu’za huyu kiumbe, bado dhiki zimkumbe,
Hapangiwi zote pembe, mipango ilo kabambe,
Hana mtu amuambe, maisha yake yatambe?

Mbona waja tusiimbe, vikaoni shida zake?
Kwa halambe na halumbe, tuchangishe pesa zake,
Yupo alo zimbezimbe, mbona waja tumwepuke?
Hana mtu amuambe, duniani apendeke?

Msiambe ni uzembe, wapo wale twawaamba,
Mitaani ukitembe, utapata wamesamba,
Alawitiwa tusambe, na tupo naye sambamba,
Hana mtu amuambe, nambie kwenyi chemba.

Kaditamati niambe, watundi tumtungiye,
Tumtoye chembechembe, awe huru pia naye,
Mwili wote tumpambe, dhiki zake tusemeye,
Hana mtu amuambe, moyo wake furahiye?

© Simon Bin Itegi

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!