Si Maziwa ni Tui

Malkia nimemaka, vimbimbi vinanitoka
Binadamu megeuka, uongo unawatoka
Wadai mekengeuka, moto mkali wawaka!

Ukiona wanacheka, usidhani wapendeka
Mafuta wanakupaka, hamnazo wakuteka
Wachache huaminika, hili limethibitika!

Mihela kiwatoka, jua kuna‘nachotaka
Sidhani wamevutika, mtegoni ‘tanasika
Utashindwa kunasuka, himahima tokatoka!

Sifo nyingi huboboka, zumbukuku hubebeka
Wapatapo walotaka, machoni wanatoweka,
Matani unawachika, daima kulalamika!

Mzigo kiupachika, ‘wataki kuwajibika
Kinyesi watakupaka, taitwa wewe kipaka
Dada yangu ‘tasagika, kamwe hutatamanika!

Ya ulevi kikupaka, kinga tasahaulika
Zinaani malizika, kama gofu utateseka
Simanzi tatugubika, kaburini takuzika!

Tausi sitaitika, kuwasuta sitachoka
Jibadili enyi kaka, wa soka nimetosheka
Kidete nimeinuka, tozi halitamwagika.

© Nyangara Mayieka

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!