Maadili

Mtima wanituama, nafsi yanisukuma
Nasakamwa natema, yote mema tayasema
Maadili kitu chema , tayatetea daima.

La mbeleni ni heshima, siyo utumwa daima
Iwe ya kwetu dhima, moyo usiwe lawama
Maadili kitu chema,  tayatetea daima.

Pili ni utu mwema, utakuhifadhi  pema
Uhayawani  takoma, hatutashikishwa tama
Maadili kitu chema, tayatetea daima.

Chuki siyo kitu chema, huliza mingi mitima
Usipende kwa kupima, fujo siwe kwa kauma
Maadili kitu chema, tayatetea daima.

Uongo wachoma, chunga usije kufuma
Mabaya mbona watema? Ki motoni chako chuma!
Maadili kitu chema, daima tayatetea.

Kaka kuwa na huruma, shida muauni hima
Mwenye bezo hebu  koma! Dunia itakutema
Maadili kitu chema, daima tayatetea.

Tamatini ninakoma, kwaherini  ninasema
Maadili zaa mema, dumisha ima faima
Maadili kitu chema, daima tayatetea.

© Nyangara Mayieka

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!