Ukeketaji

Huno ndio udhalimu, kuuharibu uke
Wakeketaji ni sumu, wawaponza wanawake
Mola atawahukumu, kukosoa kazi yake
Ukatapo kinembe, haki wazikiuka!

Huchirizi nyingi damu, kama mwehu hana lake
Makovu yatamdumu, ima akilini mwake
Utu umekuwa adimu, kaburini awaweke
Ukatapo kinembe, haki wazikiuka?

Mbona mwamtuhumu, Pasipo idhini yake?
Mmewatia ya pumu, UKIMWI mekuwa wake
Fununu zavuma humu, majanga ndoani mwake
Ukatapo kinembe, haki wazikiuka!

Lukuki mmehujumu, watesa nafsi yake
Ajifungua kwa ugumu, lilia kitoto chake
Ni nani wa kuikimu, aagapo mwanamke?
Ukatapo kinembe , haki wazikiuka!

Sote tushike zamu, kuuteteani uke
Tuipalilie hamu, kuzilinda haki zake
Tupige teke dawamu, visu nyembe wasishike
Ukatapo kinembe , haki wazikiuka!

 © Nyangara Mayieka

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!