Kukuacha

Naapa kutoadhibu, mpenzi hutoudhika,
Nitakwondoleya tabu, ukabaki wapendeka,
Nibaki wako tabibu, hino raha kukuvika,
Mrembo unapendeka, kukuacha sijaribu!

Wanambiya ya ajabu, ubongo nakanganyika,
Nishakupa langu jibu, kwa urembo wapendeka,
Miye sitoghilibu, ukweli utatendeka,
Mrembo unapendeka, kukuacha sijaribu!

Sijaipata aibu, kwa lote linatendeka,
Sikulipi kwa adhabu, kwangu unahitajika,
Ninaifanya sulubu, ukipate cha kulika,
Mrembo unapendeka, kukuacha sijaribu!

Katu sitakuwa bubu, nataka kueleweka,
Ninakupenda muhibu, wewe ni wangu rika,
Alinieleza babu, kitukuu anataka,
Mrembo unapendeka, kukuacha sijaribu!

Nahifadhi kwa vitabu, sifazo za kutukuka,
Nakupendea adabu, kwa mambo ninayotaka,
Kila swali lina jibu, jambo likihitajika,
Mrembo unapendeka, kukuacha sijaribu!

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!