Mauti

Umauti ni mlango, sisi sote tunapita
Na wala hakuna pingo, Kahari ajapokwita
Ibada ndio kilingo, adhabu usijepata
Waja wote tunapita, umauti ni mlango

Wala tusivunde shingo, tukakaa na kujuta
Ingawa twaacha pengo, mauti yakitukuta
Hima tupinde mgongo, kwa ibada na kujuta
Waja wote tunapita, umauti ni mlango

Wala usishike nyengo, umauti kuukita
Ni wa Karima mpango, yeye aliyetuleta
Sihamanike na pungo, ulipo utakufata
Waja wote tunapita, umauti ni mlango

Maisha yana uzingo, daima hutuzingata
Twaweka mengi malengo, ya halali twayaata
Tuukumbuke mlango, huo tutakao pita
Waja wote tunapita, umauti ni mlango

Tambo na yetu maringo, dunia inatuvuta
Tunajitia vifungo, akhera tutenda juta
Yatuhadaa maungo, yaso mana kuyafata
Waja wote tunapita, umauti ni mlango

Umauti ni mlango, kauweka Mtukuka
Mali na yetu majengo, hayana thamani hata
Ulio bora mpango, kwa Mola goti kukita
Waja wote tunapita, umauti ni mlango

Maasalamu mlango, wa mauti tutapita
Dua zetu ziwe kingo, tusije mbele kujuta
Yalio mkuta ungo, na kibeku humpata
Waja wote tunapita, umauti ni mlango

© Hamisi A.S. Kissamvu
Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!